14. SWAHILI — KOLLOQUIUM (Bayreuth, 25. — 27. Mai 2001)

Kusomesha Kiswahili kwa kutumia Vifaa vya Kompyuta
(Karin Geitlinger, Zurich)


Katika mada yangu ifuatayo ninayo malengo matatu. Kwanza, nataka kuwajulisha mradi ambao tunajishughulisha nao huko Chuo Kikuu cha Zurich. Mradi huo una lengo la kutengeneza masomo ya lugha ya Kiswahili kwa kutumia vifaa vya kompyuta. La pili, katika mradi huo, nitazungumzia juu ya uwezo na upungufu wa masomo haya mapya, kulinganisha na masomo ya awali. Mwisho, nitatoa baadhi ya fikira kuhusu jinsi vifaa hivyo vipya vinavyoweza kuunganishwa na mafunzo, na itakavyomhusu mfundishaji kwenye utaratibu wake.
Mradi ninaouzungumzia unaitwa ALI Swahili; ni mfuasi wa mradi mwingine uitwao ALI Akan. ALI Swahili umeanzishwa mwezi wa Oktoba mwaka uliopita, chini ya uongozi wa Pr. Bearth, na unaruzukiwa na Chuo Kikuu cha Zurich, Uswisi. Mradi huo una lengo la kutengeneza kozi ya lugha ya Kiswahili kwenye CD, na kutunga jinsi mpya ya masomo, kwa kutumia CD hiyo, pamoja na vifaa vingine vya kompyuta, hasa mtandao.
Kozi kwenye CD imepangwa kuwa na masomo 24. Kila somo litakuwa na sehemu tatu, yaani mazungumzo na maelezo ya utamaduni, sarufi, na msamiati. Kila somo litakuwa na mifano ya mazungumzo kwenye filamu au rikodi ya kusikiliza. Sampuli hizo zitakuwa msingi wa maelezo yote yatakayofuata kwenye somo moja. Vilevile, kila sehemu itakuwa na mazoezi yake. Licha ya hayo, CD itakuwa na makala kadhaa zinazoeleza mada mbalimbali kwa undani zaidi. Makala hizi zitaunganishwa na sehemu za masomo zinazohusika kwa njia ya ‚link'. Vilevile, njia hii ya ‚links' itatumiwa kuwafikisha wanafunzi kwenye sehemu za mtandao zinazohusika na mada za masomo.
Mradi wa ALI Swahili umepangwa kumudu miaka miwili. Tumetumia sura ya kwanza ya mradi huo kwa kutunga mpangilio wa yaliyomo ya masomo yote, kukusanya data, hasa kupiga picha za video na rikodi za kusikiliza, na kufanya utafiti kuhusu uwezo wa ki-technolojia. Sasa hivi tuko kwenye sura ya pili, yaani kutunga masomo yenyewe.
Mpaka leo hii tumemaliza sehemu mbili za somo la kwanza: sehemu ya mazungumzo, ambayo inatoa maelezo ya matamshi na kuhusu jinsi mbalimbali za kuamkiana na kuagana kwa Kiswahili, na sehemu ya sarufi, ambayo ina maelezo ya dhana na istilahi ya utaratibu wa ngeli. Nitatoa baadhi ya mifano kwenye maelezo yangu yafuatayo.
Kwanza, tuingie kwenye swala la manufaa ya mradi wetu: kuna vitabu chungu nzima vya kufundisha Kiswahili, kwa nini basi tunatunga masomo mengine? Sababu itakuwa wazi tukiangalia uwezekano wa chombo tunachokitumia, yaani CD, kulinganisha na chombo cha kitabu. Kwa maoni yangu, nafuu ya CD iko kwenye sehemu tatu, ambazo tunajaribu kuzisisitiza kwenye mradi wetu:
1) Uwezekano wa kutumia picha hai na sauti. Ni wazi kwamba njia bora kabisa kujifunza lugha ni kwenda kwenye nchi ambako lugha hiyo inazungumzwa, au ijapo kufundishwa na mtu ambaye ni mzungumzaji wa asili wa lugha hiyo. Lakini baadhi ya wakati, kwa sababu mbalimbali, hii haiwezekani. Hivyo basi CD itatuwezesha kupunguza tatizo hilo; yaani tunaweza kumpa mwanafunzi muktadha, ili ajifunze lugha asilia na matumizi yake yenyewe, na siyo kwa kutumia tafsiri ya lugha nyingine. Nitatoa mfano mmoja wa msamiati kusisitiza dokezo hilo: tuchukue kitenzi kuna nazi. Naweza nikamtafsiria mwanafunzi kitenzi hiki, lakini hawezi kufahamu maana yake hasa, kwa sababu kwenye mazingira yake anayoishi, watu hawakuni nazi. Lakini nikimwonyesha filamu ya mwanamke anayekuna nazi, kwa kutumia mbuzi, atakuwa na dhana ambayo itakuwa sawasawa na dhana aliyo nayo Mswahili mwenyewe akitamka kitenzi hiki kuna nazi. Na yapo maneno mengine mengi ambayo dhana zao zitafahamishwa kwa urahisi zaidi yakifundishwa kwa kutumia picha hai. Na matumizi ya sauti kwenye maelezo yanafaa kwa sababu mbili: Kwanza, yanafanya masomo yawe na uhalisi zaidi. Ya pili, yanampa mwanafunzi mifano ya matamshi moja kwa moja, ambayo anaweza kuitumia kwa kufanya mazoezi. Nitawaonyesha jinsi sauti inavyopatikana kwenye somo letu: <U01maz-e07.html>. Sehemu hii inaeleza tafauti baina ya sauti mbalimbali ambazo wanafunzi baadhi ya wakati wanapata taabu kuzitamka sawasawa. Kwa kubonyeza kwenye mifano yenyewe wanapata sauti hizo, mara zozote watakazo.
2) Sehemu ya pili ambapo chombo cha CD kinafaa kuliko kitabu ni matumizi ya mifano hai. Kwa upande mmoja hii inaweza kutumika kwenye maelezo, hasa maelezo ya sarufi. Inaweza kupangwa ili msomaji apate umuhimu wake hatua kwa hatua, kwa kuchunguza mwenyewe; yaani, tunamtaka mwanafunzi ashiriki kwenye kujipatia ujuzi, siyo akae tu asome. Kwenye kozi yetu tunatumia sana rangi kuongeza uhai wa maelezo na mifano yake; kwa kusukuma kipanya, mwanafunzi anaweza kupeleleza undani wa mifano, na uhusiano baina ya maelezo na mifano. Mifano miwili ifuatayo, kutoka somo letu, inaonyesha sifa ya uhai inavyotumilika: <U01maz-e33.html> Mfano wa kwanza unatoka kwenye maelezo juu ya maamkio. Inaelezwa kwamba maamkio yana sehemu nne mbalimbali. Kwa kusukuma kipanya, inawezekana kupata wazi mgawanyo baina ya sehemu hizo na sehemu za mazungumzo yanayohusika. Mfano wa pili unatoka sehemu ya sarufi: <U01sar-e17.html>. Hapa mwanafunzi anapewa maelezo ya umilikifu wa ngeli nomino kwenye sentensi. Baada ya kubonyeza na kupata mifano, anaweza kuona viambishiawali vya ngeli kwa kusukuma panya juu ya mifano hiyo. Ikisha anaweza kuona uhusiano baina ya aina za maneno na maneno ya mifano yenyewe. Sifa ya mifano hai ina faida kubwa kwenye mazoezi vilevile: badala ya kupata majibu sahihi moja kwa moja, mwanafunzi anaweza kujaribu tena akiwa amekosea, na anaweza kupata madokezo akikwama. Vilevile, mwishoni mwa kila zoezi atapata matokeo ya utendaji wake, ambayo yatamsaidia kujipima mwenyewe, na yatamsaidia mwalimu kuwapima wanafunzi wake.
3) Sehemu ya tatu ya manufaa ya CD ni uwezekano wa kuunganisha sehemu mbalimbali kwa njia ya ‚link'. Hii inatupa nafasi kuchangia maarifa ya ziada bila ya kufumba maelezo ya msingi. Kwa mfano: kwenye maelezo ya ngeli tunaweza kuunganisha makala kuhusu semantiki ya ngeli, kuhusu ushiriki wa maneno ya mkopo kwenye utaratibu wa ngeli, na vinginevyo. Mwanafunzi anaweza kuyasoma makala haya kwa hisani yake, na baada ya mzunguko atarudi moja kwa moja kwenye barabara kuu, yaani maelezo ya msingi, bila ya kupotea kwenye wingi wa maarifa. Vilevile, michango ya ziada siyo lazima iwemo kwenye CD yenyewe; hata makala ambazo zimo kwenye mtandao zinaweza kuunganishwa na kozi kwa njia ya ‚link'. Hatujapata nafasi kutia makala ambazo ziko nje ya kozi, kwa hivo itabidi niwaonyeshe ‚links' zinavyofanya kazi kwenye utaratibu mwingine tunaoutumia: <U01maz-e53.html> Mwishoni mwa kila sehemu kuna muhtasari ya maelezo maalum ya sehemu hiyo. Kwa kutumia njia ya ‚links' kwenye muhtasari hizo tunampa nafasi mwanafunzi kuzitizama tena sehemu ambazo hajazifahamu.
Hizo ndizo faida kuu za CD kulinganisha na kitabu.

Juu ya hayo, kuna faida kadhaa za masomo ya CD kulinganisha na masomo ya uso kwa uso, yaani darasani. Nitazitaja mbili:
1) Faida ya kwanza ni kwamba anayeamua kasi ya masomo si mwalimu, bali ni mwanafunzi mwenyewe; yaani ikiwa mwanafunzi hajafahamu sehemu moja ya maelezo, anaweza akasimama hapohapo kuyachunguza zaidi hayo maelezo na mifano yake. Anaweza hata akarejea na kupata maelezo zaidi kwa njia ya ‚links', mpaka afahamu. Darasani haiwezekani kumjaalia kila mwanafunzi kwa kuwa kila mwanafunzi ana ufahamu wake.
2) Faida ya pili, ambayo inatokana na faida ya kwanza, ni kwamba wanafunzi wa vyeo mbalimbali wanaweza kufundishwa kwa kutumia CD hiyo moja. Kwa mfano, kwenye kozi, maelezo ya sarufi yanaweza kutungwa kwenye lugha rahisi, bila ya kutumia istilahi au dhana nyingi za isimu. Hivo hata mtu ambaye si mtaalamu wa lugha anaweza kuyafahamu masomo na anaweza kuyatumia kujifunza lugha hiyo. Na wakati huohuo tunaweza kumridhisha mwanaisimu: yeye atakuwa na nafasi kufuata njia nyingine kwenye kozi hiyo hiyo, kwa kutumia utaratibu wa ‚link'. Darasani haiwezekani kufuata njia mbili hizi; kila ukichukua kikundi kimoja cha wanafunzi, utakiacha kingine.
Kwa kusema hivyo basi, sina maana kuwa masomo ya CD, yanavyopangwa kwenye ALI Swahili, yanakusudiwa kuchukua nafasi ya masomo darasani. Hatukusudii kompyuta kuchukua nafasi ya mwalimu, wala hiyo haiwezekani. Ukiacha faida ambazo nimekwisha kuzitaja, zipo kasoro mbalimbali za kujisomea mwenyewe, tukilinganisha na utaratibu wa kufundishwa darasani. Nitazitaja kasoro tatu ambazo zote zinatokea endapo mwanafunzi atajisomea mwenyewe bila ya mwalimu:
1) Hata ikiwa mifano hai itarahisisha ufahamu, mara nyingi mwanafunzi atakuwa na maswali ambayo lazima ajibiwe kabla hajaweza kufahamu maelezo kwa ufahamu wake. Na maswali hayo hayatajibika kwa kompyuta. Mtungaji wa masomo, kwa uzoefu wake wa kufundisha, anaweza akajua baadhi ya maswali ambayo yataulizwa, na anaweza kuyaingiza kwenye maelezo yake; lakini hawezi kuyajua maswali yote. Hapo itakuwa lazima kuwa na mwalimu ambaye atajibu maswali na kuwasaidia wanafunzi ana kwa ana.
2) Kasoro ya pili inahusu matamshi. Kwa kutumia sauti kwenye masomo, tunampa mwanafunzi nafasi kufananisha matamshi yake na matamshi ya mzungumzaji wa asili. Hivyo anaweza kurekebisha matamshi kwa uamuzi wake yeye. Lakini uamuzi huo unaweza kuwa tafauti na uamuzi wa mzungumzaji wa asili anaposikia matamshi hayo; yaani mwanafunzi anaweza akakosea ki-matamshi bila yeye mwenyewe kutambua. Kwa hivyo itakuwa lazima akutane na mzungumzaji wa asili, au mtu mwenye uzoefu wa kuzungumza lugha hiyo, arekebishwe matamshi yake.
3) Kasoro kubwa ya tatu ni kwamba kompyuta haiwezi kumzungumzisha mwanafunzi; yaani hata ikiwa nafasi zipo kwa mwanafunzi kutumia ujuzi wake ki-bunifu, kwa kutunga sentensi mwenyewe au kuchangia kwenye mazungumzo, hakuna uhakika kwamba kweli atazitumia nafasi hizo. Kwa uzoefu wangu wa kufundisha najua kwamba kuna tafauti kubwa baina ya kujifunza lugha na kusema lugha; mara nyingi mwanafunzi anajua lugha kinadharia, lakini anashindwa kuchangia kwenye mazungumzo kwa sababu anaona haya kutumia lugha anayojifunza. Haya hiyo inaweza kupunguzwa darasani tu, kwa kumlazimisha mwanafunzi azungumze tangu mwanzoni.

Tukishajua faida na kasoro za vifaa vya kompyuta kwenye kufundisha lugha, itabidi tuviunganishe na taratibu za awali kwa namna ambayo inaongeza faida na kupunguza kasoro za kila chombo. Kutokana na nia hiyo, katika mradi huo wa ALI Swahili masomo yatapangwa kwenye sura tatu, ambazo zitaingiliana:
1) Masomo ya nafsi kwa kutumia CD. Maelezo mengi mwanafunzi atajisomea mwenyewe, kwa mwendo wake, kwa kufuata masomo ya CD na makala ya ziada. Atapewa ratiba ambapo amepangiliwa hatua zake, yaani muda anaoweza kuutumia kwa kila somo.
2) ‚Madarasa ya mtandao'. Licha ya kujisomea mwenyewe, mwanafunzi atapewa nafasi kuwasiliana na wanafunzi wenzake na mwalimu. Nafasi hii itatumia vifaa vya mtandao, hasa barua za umeme na ‚chumba cha mazungumzo', yaani ‚chat room'. Vifaa hivyo vitaongozwa na mwalimu: yeye atatoa mazoezi au mada ambazo zitazungumzwa kwenye ‚chat room', na atajibu maswali ambayo yatamfikia kwa barua za umeme. Ikitakiwa, mwanafunzi anaweza kupewa wakati au muda maalum ambapo lazima awemo kwenye mtandao; teknolojia za kompyuta zinamwezesha mwalimu hata kukagua kama mwanafunzi anatimiza wajibu huo.
3) Madarasa ya ‚uso kwa uso'. Baadhi ya wakati mwalimu atakutana na wanafunzi wake darasani kama kawaida. Lakini yaliyomo ya madarasa yatabadilika. Kwa sababu mwanafunzi atakuwa ameshajisomea maelezo mengi kwa kutumia CD, mwalimu atakuwa na nafasi ya kufundisha mengine badala yake. Hapo itakuwa vizuri kusisitiza vipengele ambavyo ni vigumu kufundishwa kwa njia ya CD: kwa mfano matamshi, mazungumzo, ufahamu wa kusikiliza, na kadhalika. Vilevile, kutokana na mawasiliano kwenye mtandao, mwalimu atajua baadhi ya matatizo waliyo nayo wanafunzi, na ataweza kupanga masomo darasani kulingana na matatizo hayo. Na muda ukibaki, anaweza kuzungumzia baadhi ya matini kwa undani zaidi.
Mpangilio huo unaonyesha kwamba vifaa vya kompyuta, vilivyotajwa kwenye maelezo yangu, hayakusudiwi kuchukua nafasi ya mwalimu. Lakini itabidi mwalimu abadilishe utaratibu wake wa kufundisha: badala ya kutayarisha masomo ya sarufi, ya kufundishwa darasani, kazi yake kubwa itakuwa kuwasiliana na wanafunzi kwa njia ya mtandao, ambapo atawapa mazoezi na kuyasahahisha, pamoja na kujibu maswali ya wanafunzi. Vilevile, mwalimu atatakiwa awe na uwezo wa kubadilisha mipangilio ya mafunzo kulinganisha na mahitaji ya wanafunzi. Mahitaji hayo yatajulikana kutokana na mawasiliano mtandaoni.
Bila ya shaka hii itaongeza kazi yetu sisi walimu. Lakini vilevile, itaifanya kazi hiyo iwe ya kuvutia zaidi, kwa sababu itakuwa na sura mbalimbali. Na nina uhakika kwamba ikiwa nia yetu ni kufundisha lugha kama jambo hai, kama chombo cha uhusiano baina ya watu, basi vifaa vya kompyuta vitatuzalia matunda mengi katika kazi hiyo.
Kuwepo kwa kompyuta kwenye sehemu mbalimbali za maisha ya kila siku si swala la upendo, bali ni swala la lazima na la uhakika siku hizi. Kwa hivo tusifumbie macho jambo hili, bali tulichunguze na kulitumia ipasavyo ili kufaidisha malengo ya kazi yetu.

SPW/ afrling/ALI Swahili/ Project   prev  up  next